Jumanne, 21 Aprili 2015

Wazazi fuatilieni watoto wenu wasome - Magufuli.

Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, 


Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, amewahimiza wazazi na walezi nchini kuwasimamia vizuri watoto wao katika masuala ya elimu ili kuwaepusha na matendo maovu katika jamii.
 
Dk. Magufuli alitoa kauli hiyo wakati wa mahafali ya 10 ya kidato cha sita katika shule ya Sekondari ya Chato mkoani, Geita ambayo jumla ya wanafunzi 84 wanatarajia kuhitimu.
 
 “Wazazi mnatakiwa kuhakikisha mnawafuatilia watoto wenu katika masomo yao na kuacha tabia ya kutoa uhuru mkubwa ambao hutumika vibaya. 
Inabidi muwabane sana hata wakichukia leo, kesho watakuja kufurahi na kuona faida yake,” alisema Waziri Magufuli.
 
Kadhalika, Dk Magufuli aliwaasa pia wanafunzi wa kidato cha kwanza mpaka cha nne kuhakikisha kuwa wanasoma kwa bidii ili wafaulu kuingia kidato cha tano“Mnatakiwa kuanzia sasa kupanga mikakati mizuri ya kujisomea kwa muda huu uliobaki na kwa mwaka huu kusiwe na daraja la nne katika matokeo yenu,” alisema Dk. Magufuli
 
Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Sekondari Chato, Hellen Busumilo, aliwahimiza wazazi kusaidiana na walimu katika malezi ya watoto na mtoto anapokosea aadhibiwe kwani kwa kutofanya hivyo ni kosa litakalosababisha watoto kufanya matendo maovu.
 
“Usimamizi wa watoto ni jukumu la wazazi wote, mzazi nyumbani na mwalimu shuleni ili tuwasaidie watoto wetu hasa watoto wa kike,” alisema Busumilo.
 
Mkuu wa shule hiyo, Mwalimu Mafere Mahendeka, alimshukuru Dk Magufuli, ambaye pia ni Mbunge wa Chato kwa kuhudhuria mahafali hayo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni