![]() |
Rita Jeptoo, mwanariadha wa Kenya anayetumikia adhabu ya kufungiwa miaka miwili kwa kosa la kutumia dawa zakuongeza nguvu michezoni |
Mwanariadha maarufu nchini Kenya Rita Jeptoo anaweza kuongezewa adhabu zaidi endapo Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Riadha, duniani, IAAF, litamtia hatiani zaidi kutokana na kosa la kutumia dawa za kuongeza nguvu michezoni zilizopigwa marufuku.
Jeptoo kwa sasa anatumikia adhabu ya miaka miwili.
Shirikisho hilo la IAAF limekata rufaa katika mahakama ya michezo (CAS) likidai kuwa adhabu iliyotolewa dhidi ya Jeptoo ni ndogo sana.
Kwa upande wake, Jeptoo amekata rufaa dhidi ya adhabu hiyo na pia anaitaka mahakama ya CAS imruhusu kuendelea kukimbia wakati suala hilo linashughulikiwa.
Jeptoo alifungiwa kushiriki michezo ya riadha baada ya kukutwa akitumia dawa ya kuongeza nguvu michezoni iliyopigwa marufuku aina ya EPO.
Adhabu hiyo ilitolewa na tume ya kupinga matumizi ya dawa za kuongeza nguvu michezoni ya chama cha riadha cha Kenya.
Hiyo ilikuwa adhabu ya chini kwa mujibu wa sheria za kimataifa za kupinga matumizi ya dawa za kuongeza nguvu michezoni wakati alipogundulika katika uchunguzi wa kitabibu wa matumizi ya dawa hizo mwaka jana.
Hata hivyo, wanariadha waliokamatwa wakitumia dawa za kuongeza nguvu michezoni mwezi Januari mwaka huu wanakabiliwa na adhabu ya miaka minne kutoshiriki michezo ya riadha.
CAS imetangaza Jumanne kwamba imepokea rufaa mbili juu ya suala hilo.
"Katika rufani yake kwa mahakama ya CAS, Bi Jeptoo anaomba kuwa uamuzi unaopingwa uwekwe kando na kwamba afutiwe adhabu ya miaka miwili," imesema CAS katika taarifa yake.
Wakati huo huo, taarifa hiyo imesema: " Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Riadha (IAAF) pia limetuma ombi, likiomba kuwa kipindi cha kufungiwa kwa mwanariadha anayekutwa na kosa hilo kiongezwe hadi miaka minne.
Maombi yote mawili "yanashughulikiwa kwa mujibu wa kanuni za michezo," imesema CAS.
Jeptoo, mshindi wa mashindano ya mbio za marathon za Boston na Chicago, ni jina lenye hadhi ya juu kabisa miongoni mwa wanariadha wa Kenya kukamatwa na kosa la udanganyifu michezoni na kashfa hii imetia doa katika mafanikio iliyopata Kenya katika mbio za masafa marefu.
Tayari amenyimwa tuzo ya dola 500,000 za Kimarekani kwa kushinda mataji ya dunia ya mbio za marathon zilizopita.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni