Ijumaa, 3 Aprili 2015

PAMOJA NA KUAIRISHWA TAREHE YA KURA YA MAONI, UMOJA WA MATAIFA WAFADHILI USAMBAZAJI WA KATIBA INAYOPENDEKEZWA KWA NJIA YA SAUTI.



Pamoja na Tume ya  Taifa ya Uchaguzi kuahirisha  tarehe ya kupiga kura ya maoni, Shirika la Kimataifa linaloshughulikia Elimu na Utamaduni (UNESCO), kwa kushirikiana na Kampuni ya Focus Media pamoja na Mtandao wa radio za jamii  (COMNETA), limeamua kusambaza Katiba inayopendekezwa kwa njia ya sauti nchi nzima, ili wananchi wapate elimu  kuhusu maudhui yaliyomo ndani ya Katiba na kufanya maamuzi sahihi pindi siku ya kupiga kura itakapowadia.
Aidha, mkakati huo wa kusambaza Katiba inayopendekezwa kwa njia ya sauti unajumuisha utoaji elimu kuhusu mfumo mpya wa kujiandikisha kwa njia ya kieletroniki (Biometric Voters Registration – BVR) pamoja na kuhamasisha wananchi ili wajitokeze kwa wingi kujiandikisha na kutimiza haki yao ya kikatiba wakati wa upigaji kura.

Akipokea, nakala za CD zenye Katiba inayopendekezwa kwa njia ya sauti, Mkurugenzi Mkaazi wa UNESCO nchini Tanzania Bi Zulmira Rodrigez, alipongeza Kampuni ya Focus Media kwa kuandaa matoleo hayo na kusisitiza radio za jamii kuzitumia ili kuwaelimisha wananchi mikoa yote juu ya Katiba inayopendekezwa.

Mwenyekiti wa mtandao wa redio za jamii Bwana Joseph Sekiku amewashuri watangazaji wa redio mbalimbali waliohudhuria semina hiyo kuelimisha jamii maudhui ya Katiba inayopendekezwa ili wananchi wafanye maamuzi sahihi katika kura ya maoni na uchaguzi mkuu.


Sekiku ameongeza kwamba kwa sasa itapatikana kupia Focus Media pro ltd kwa kupitia mitandao yote ya kijamii na redio mtandao na wananchi wanaweza kuwasiliana kwa kutuma ujumbe mfupi kupitia namba  +255 (0)772 55 55 53

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni