NAIBU Waziri wa Nishati na Madini,
Dkt Medard Kalemani amezindua Mradi
wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA
III) katika Mkoa wa Simiyu ambapo
vijiji 347 mkoani hapo vipata
nishati hiyo.
Uzinduzi huo ulifanyika juzi
katika Kijiji cha Nangale ,Kata ya
Ndolelezi wilayani Itilima na kuhudhuriwa na viongozi
mbalimbali wa Serikali, Wabunge na
wananchi wa mkoa wa Simiyu.
Naibu Waziri alitaja lengo jingine
la REA III kuwa ni kupeleka umeme
kwenye vijiji vyote ambavyo
havijapata umeme sambamba na hayo
alibainisha malengo mengine kuwa ni
kupeleka umeme kwenye Taasisi zote
za umma na nyingine zilizo rasmi
hata kama siyo za umma.
“Taasisi hizo ni pamoja na Vituo vya
Afya na Zahanati, Shule pamoja na
Taasisi nyingine muhimu pia kwenye
miundo mbinu ya maji ambayo ni
mitambo ya maji,” alifafanua.
Akizungumza na wananchi mara
baada ya uzinduzi, Dk Kalemani
alibainisha malengo ya REA III
ambapo alisemaa lengo la kwanza la
Mradi huo kabambe ni kupeleka umeme
kwenye vitongoji vyote .
“Katika Mradi wa REA II tulikuwa
tunapeleka umeme katika Kituo tu cha
Kijiji, siyo Kijiji chote REA
III itafika katika vitongoji
vyote.”alisema huku akishangiliwa na
wananchi waliohudhuria hafla
hiyo.
Pia aliwashukuru wananchi kuitikia
Mradi huo wa Serikali ambao
alibainisha kuwa utatekelezwa ndani
ya kipindi cha miaka minne ambapo
katika awamu ya kwanza mradi huo
utatekelezwa katika vijiji 152 kwa
kipindi cha miezi 24 na vijiji
vingine vilivyobaki 195 navyo
vitapatiwa umeme kwa kipindi kingine
cha miezi 24.
Hata hivyo aliwataka wananchi
kuutumia umeme watakaounganishiwa
katika shughuli mbalimbali za
kiuchumi.
“Tunapenda sana umeme huu utumike
kwenye shughuli za kilimo hususan
kilimo cha umwagiliaji, kuendeshea
mitambo ya maji, lakini hata
kuanzisha viwanda vya kati ili
kukuza uchumi wetu tunaamini kuwa umeme
huu utakuwa kichocheo kikubwa katika
kusukuma maendeleo,” alisisitiza.
Vilevile, Naibu Waziri alibainisha
kuwa lengo la Serikali ni kuwapatia
wananchi wote umeme pasipo kubagua
aina ya makazi wanayoishi.
“Mahali popote mwananchi anapoishi,
ndipo tutakapomtundikia umeme.
Hatutajali ni nyumba ya nyasi au ya
ghorofa.”alisema
Kupitia uzinduzi huo, Naibu Waziri
aliwatambulisha kwa wananchi na
viongozi wa mkoa Wakandarasi
wawili ambao ni White City
International Contractors na Guang
Dong Jianneng Electiric Power
Engineering Co Ltd watakaotekeleza
Mradi huo ili kurahisisha
ufuatiliaji wa utekelezaji wa kazi
zao pamoja na kuwapatia ushirikiano
stahiki.
Dkt Kalemani alitoa angalizo kwa
Wakandarasi hao na kuwataka kuwatumia
wakandarasi wasaidizi wenye uwezo
waliko ndani ya Mkoa wa Simiyu huku
akipiga marufuku kuingiza nguzo na
transfoma kutoka nje ya nchini
sambamba na Shirika la Umeme Nchini
(Tanesco) kuwasimamia katika kazi
Usiku na Mchana ili kuhakikisha kuwa
mradi huo unaisha kwa wakati
uliopangwa.
Awali, akitoa hotuba ya utangulizi
katika hafla hizo za uzinduzi,
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati
Vijijini (REA), Mhandisi Gissima
Nyamo-Hanga aliwataka wananchi
watakaounganishiwa umeme kukamilisha
utandazaji wa nyaya katika nyumba
zao mapema ili mkandarasi
atakapofika katika maeneo yao wawe
tayari kulipia na kuunganishiwa
umeme.
Aidha alibainisha kwamba kwa nyumba
ambazo utandazaji wa nyaya utakuwa
haujakamilika, wananchi wanaweza
kuomba kufungiwa kifaa cha Umeme
Tayari (UMETA) ambacho hakihitaji
nyumba nzima kutandazwa waya.
Mhandisi Nyamo-Hanga aliwaomba
watendaji katika Serikali za Kata na
Vijiji, kubainisha maeneo maalum ya
viwanda ambayo katika mradi huo
yatafikishiwa miundombinu ya umeme
mkubwa ili kuwezesha wajasiriamali
vijijini kupatiwa umeme
utakaowezesha kuanzishwa kwa viwanda vidogo
vidogo na vikubwa vijijini kwa
gharama nafuu.
Gharama ya utekelezaji wa Mradi wa
REA III kwa Mkoa wa Simiyu ni
shilingi bilioni 33.47.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni