SERIKALI Mkoani Simiyu yajipanga kwa
kuweka mkakati utakaowasaidia wafugaji mkoani humo kufugaji kisasa kwa ufugaji wenye tija.
Aidha imedhamiria kuwatambua
wafugaji wote, maeneo yao na kuwaelemisha kuhusu upimaji wa maeneo hayo ili
wayatumie kufuga kisasa badala ya kuhama hama kufuata maji na malisho katika
mikoa mingine.
Serikali mkoani hapo kupitia wataalam wa
kilimo na mifugo watatoa elimu kwa Wafugaji watakaorasimisha maeneo yao, ili
wayatumie kupata malisho ya mifugo na kuweka miundombinu muhimu ya mifugo kama
majosho na visima katika kukabiliana na changamoto ya upungufu wa malisho na
maji.
Hayo yalibainishwa na Mkuu wa Mkoa
wa Simiyu katika kikao maalum ambacho kimewahusisha viongozi wa Serikali,
viongozi wa dini, wafugaji,wataalam na wadau mbalimbali wa mifugo kutoka ndani
na nje ya mkoa kilichofanyika katika Ukumbi wa Kanisa Katoliki mjini
Bariadi.
“Hatuwezi kuwa Serikali ambayo ina
majibu mepesi kwenye mambo ya msingi,lazima tupate majawabu ya wafugaji ndani
ya mkoa wetu, tufike mahali ambapo mfugaji kutoka mkoa wa Simiyu hatapigwa
faini kwenye mikoa mingine kwa sababu ya kutafuta maji na malisho”amesema Mtaka
Aliongeza kuwa Mkoa unaandaa
utaratibu ambapo shule za Serikali zitakapokuwa zinafungwa, idara ya kilimo na
mifugo itatumia madarasa hayo kutoa elimu ya ufugaji na kilimo bora kwa
wananchi.
Hata hivyo alisema zoezi la kupima maeneo ya wafugaji na
kuweka miundombinu muhimu ya mifugo litakapokamilika Serikali imepanga kuweka
mizani katika minada yote mkoani humo ili wafugaji wasidanganywe na kuibiwa
wanapouza mifugo yao.
Kwa upande wake Daktari wa Mifugo wa
Sekretarieti ya Mkoa wa Simiyu, Gamitwe Mahaza alisema baadhi ya wafugaji ni wakulima, hivyo ni vema wakatumia masalia
ya mazao kwa ajili ya malisho badala ya kuyaacha mashambani huku akasisitiza juu ya urasimishaji wa maeneo yao
ili miundombinu kama visima iwekwe kusaidia ukuaji wa malisho ya asili na
upandaji wa malisho ya kisasa.
Naye Mtaalam wa Mifumo ya TEHAMA
kutoka Tume ya Sayansi na Teknolojia(COSTEC), Mhandisi George Mulamula ameeleza
kuwa upimaji katika maeneo ya wafugaji unaweza kufanyika kwa kutumia njia
mbalimbali zikiwemo zinazotumia mifumo ya TEHAMA , kama vile matumizi ya
satelite na ndege zisizotumia rubani ambazo zitasaidia zoezi hilo
kufanyika kwa haraka.
Mkoa wa Simiyu ni moja ya mikoa
inayoongoza kwa kuwa na mifugo mingi hapa nchini, hali inayopelekea baadhi ya
wafugaji kuhamia maeneo mengine ili kutafuta malisho, hivyo Serikali imedhamiria
kuona wafugaji mkoani humo wanahama kutoka kwenye kufuga kwa mazoea na kuingia
kwenye ufugaji wa kisasa wenye tija.
Na ANITA BALINGILAKI
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni