MBUNGE wa Jimbo la Itilima Njalu
Silanga ameiomba wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
kuhakikisha inaleta wataalamu wa idara ya afya ili kuweza kutoa huduma stahiki
katika jengo la upasuaji kata ya Nkoma lililofunguliwa juzi na Rais mstaafu
Mkapa.
Njalu alisema kuwa pamoja na
kukamilika kwa jengo hilo upungufu wa watumishi bado ni changamoto kubwa na
wajibu wa serikali ni kuajiri watumishi ili waweze kuhudumia wananchi kwa
mujibu wa sera ya afya .
Aliyasema hayo juzi wakati Taasisi
ya Mkapa foundation ikikabidhi jengo la upasuaji katika kata ya Nkoma wilayani
Itilima mkoani simiyu ili kunusuru maisha ya wagonjwa ambao awali hawakuwa na
huduma hiyo ya upasuaji.
‘’nikuombe mheshimiwa waziri wa afya
kuhakikisha unaangalia upatikanaji wa wataalamu ili wakinamama hawa waweze
kujifungua salama…lakini pia tutashirikiana na wananchi kuhakikisha tunatunza
miundombinu iliyowekwa hapa ili iweze kudumu kwa kushirikiana na wataalamu’’
alisema Njalu.
Aliongeza kuwa wilaya ya Itilima ina
vituo vya afya vitatu na zahanati 23 lakini watumishi wa idara hiyo wamekuwa
hawakidhi mahitaji ya wananchi wanaofika
kupata huduma.
Mbunge wa Jimbo la Itilima Njalu
Silanga akiwapongeza taasisi ya Mkapa foundation kwa kujenga na kukabidhi jengo
la Upasuaji kata ya Nkoma wailayani Itilima Mkoani Simiyu jana.
|
Kwa upande wake waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu alisema kufikia
Desemba mwaka huu serikali italeta mashine ya ultra sound ili
kuweza kukidhi mahitaji ya wagonjwa, na pia wataajiri zaidi ya watumishi wa
afya 3000 na kupunguza changamoto ya uhaba wa watumishi wa afya.
Mwalimu alisema kuwa serikali
itaendelea kutatua changamoto za afya hasa huduma ya upasuaji ili kufuikia 2020
angalau 50% ya vituo vya afya vitoe huduma ya upasuaji ili kuokoa maisha ya
wagonjwa.
Aliongeza kuwa vifo vitokanavyo na
uzazi kati ya wakina mama 100,000 vimepungua kwa mwaka hadi 559 kwa mwaka
ambavyo husababishwa na kuvuja damu, maambukizi ya maradhi na uzazi pingamizi.
Katika hatua nyingine Mwalimu
amesema kuwa serikali imetoa bei elekezi kwa dawa za binadamu ili hata
mwananchi mwenye kipato kidogo aweze kumudu gharama za matibabu huku
akisisitiza kuwa dawa siyo bure.
“Hatutoi dawa bure na wananchi mnatakiwa kuchangia dawa
katika vituo na zahanati…bei za dawa zimepunguzwa tunataka wananchi waone
upungufu huo ” alisema Mwalimu.
Jengo hilo ambalo limejengwa na
taasisi ya Mkapa Foundation kwa kushirikiana na nchi ya Japan limegharimu
milioni 270 ambapo litaweza kuhudumia wakinamama wajawazito wenye uzazi
pingamizi, na wagonjwa wengine ambapo awali walikuwa wakiipata huduma hiyo
umbali wa kilomita 40 katika wilaya ya Bariadi.
Wananchi waliohudhuria katika
ufunguzi huo walisema kuwa jengo hili limeongeza faraja kwa akinamama
wajawazito waliokuwa wakipata uzazi pingamizi na wagonjwa kwani wengi wao
walikuwa wakifia njiani wakati wakisafirishwa kwenda hospitali ya Somanda
kupata huduma ya upasuaji.
Ufunguzi wa jengo hilo ulihudhuriwa
na Rais mstaafu wa awamu ya tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Benjamini
Mkapa .
Na ANITA BALINGILAKI
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni