Jumapili, 9 Julai 2017

MKAPA:TUAMKE TUSITARAJIE MATAIFA KUTUINUA WAKATI TUMEKAA.



Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Benjamina Mkapa akikata utepe kuashiria ufunguzi wa jengo la upasuaji katika kata ya nkoma walayani Itilima mkoani simiyu, kulia kwake ni waziri wa Afya, Maendeleleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto Mhe. Ummy Mwalimu na kushoto kwake ni balozi wa japan nchini Tanzania Masaharu Yoshida pembeni ya balozi ni mkuu wa mkoa wa simiyu Antony Mtaka.



RAIS wa Awamu ya tatu Benjamini mkapa amewataka watanzania kujitegemea kwa kubuni miradi itakayosadia jamii kwa lengo kuondokana na utegemezi wa mataifa tajiri.

Mkapa alisema kuwa kama taifa tusitarajie mataifa tajiri kuja kutuinua kama sisi wenyewe tumekaa kwani ni dhana potofu inayorudisha nyuma juhudi za maendeleo kwa wananchi.

Aliyasema hayo wakati akifungua jengo la upasuaji katika kata ya Nkoma wilayani Itilima mkoani Simiyu ambalo limejengwa na taasisi ya Mkapa Foundation kwa kushirikiana na nchi ya Japan .

Jengo hilo limegharimu shilingi  milioni 270 ambalo litasaidia wagonjwa hususani kina mamawajawazito kupata huduma hiyo karibu kwa awali walitembea umbali wa kilomita 40 kufata huduma hiyo.


Aliongeza kuwa kila mtanzania ana wajibu wa kuhakikisha taifa linajitegemea na kuwaletea wananchi wake maendeleo, huku akiwataka wasomi na wafanyakazi kuendesha midahalo na makongamano ya kuhakikisha nchi inajitemegea.


“ kila siku utasikia watu wanadai haki, makongamano, midahara ya kudai haki, swali la kuwauliza wao je wametimiza wajibu kama watanzania? Maana hakuna haki bila wajibu, ni lazima kubadilika na kuendesha makongamano ya kuonyesha nchi itajitegemea vipi” alisema Mkapa.

Aidha ameongeza kuwa ili kuweza kujitegemea ni lazima kila mtanzania akatimiza wajibu wa kufanya kazi kama Rais Magufuli anavyosema, huku akitoa mfano katika nchi ya Japani kuwa wananchi wake jambo la kwanza ni kufanya kazi.
 
Rais wa awamu ya Tatu Benjamini mkapa akikagua vitanda ndani ya jengo la upasuaji baada ya ufunguzi wake katika kituo cha Afya nkoma wilayani Itilima mkoani Simiyu



“ kama tunatarajia mataifa kuja kutuinua wakati sisi tumekaa, ni dhana potofu, viongozi tubuni miradi ili tujiendeleze na kujiletea maendeleo sisi wenyewe, kama nchi ya Japani wanavyofanya” alisema Mkapa.

Aliongeza kuwa toka utawala wa Baba wa Taifa na sera ya Chama cha Mapinduzi toka zamani ilikuwa ujamaa na kujitegemea, jambo ambalo ameeleza lazima litekelezwe kwa kila mmoja katika kutimiza wajibu kwa nafasi yake.

Akiongelea Jengo hilo Mkapa ameishukuru nchi ya Japana ambao walitoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa jengo hilo kupitia taasisi ya Mkapa foundation, huku lengo likiwa kupunguza vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga.

“ Nchi yetu bado tunakabiliwa na changamoto ya vifo vya akina mama wajawazito pamoja na watoto wachanga, Nchi ya Japan wametoa msaada huo kwa ajili ya kukabiliana na changamoto hii, taasisi ya Mkapa foundation itaendeleza ushirikiano na serikali katika kutatua changamoto mbalimbali za afya” alisema Mkapa.



Rais Mtaafu wa awamu ya tatu Benjamini Mkapa akipata maelelzo toka kwa mtaalamu wa afya jinsi kituo hicho kitakavyotoa huduma kwa wananchi mara baada ya kufungua jengo la upasuaji katika kituo cha afya nkoma wilayani itilima mkoani simiyu


Kwa upande wake mbunge wa Jimbo la Itilima Njalu Silanga amesema kuwa pamoja na kukamilika kwa jengo hilo bado kuna upungufu wa watumishi hivyo  kuiomba  serikali  kuajiri watumishi ili waeze kuhudumia wananchi.


Nao baadhi ya wananchi waliohudhuria ufunguzi huo wamesema jengo hilo limeongeza faraja kwa akinamama wajawazito kwani baadhi yao walikuwa wakifia njiani wakati wakisafirishwa kwenda Bariadi kupata huduma ya upasuji.

Na ANITA BALINGILAKI

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni