
baadhi ya wakaazi waliokumbwa na mafuriko
MAWASILIANO katika barabara kuu Kyela Mjini kuelekea Mji wa Ipinda hadi Matema yamekatika ,kutokana na mafuriko ambayo yamesababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha Mkoani Mbeya ,wakati huo shule nane za msingi na sekondari zikifungwa baada ya kujaa maji na nyingine wanafunzi kukosa mahali pa kupita kutokana na mafuriko hayo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maafa Wilaya ya Kyela na ndiye Mkuu wa Wilaya ya hiyo, Dk Thea Ntala ametoa amri ya kufunga shule tano za msingi na tatu za sekondari ambazo ni Mwaya , Bujonde na Kajunjumele baada ya baadhi ya shule hizo kujaa maji na nyingine wanafunzi kushindwa kupita baada ya madaraja ya mito wanayovuka kujaa maji, Pia ameiomba serikali kuisaidia Halmashauri hiyo tani tano za chakula kwaajili ya tahadhari japokuwa kuwa kwa sasa Wilaya hiyo haina njaa.
Pamoja na haya Mkuu huyu wa Wilaya amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Clemence Kasongo, kumchukulia hatua Mkuu wa Shule ya Sekondari Mwaya kutoka na uzembe wa kusababisha vitendea kazi vya shule hiyo zikiwemo Komputa na vitabu kulowana bila kuchukua tahadhari huku akijua kuwa shule hiyo kila mwaka inakumbwa na mafuriko.
Baadhi ya Wananchi wa Wilaya ya Kyela wameiomba serikali kuinua barabara ya kutoka Kyela mjini kuelekea miji ya Ipinda na Matema ili kuepusha adha ya kukatika kwa mawasiliano.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni