Meneja wa Kituo cha Habari na Mawasiliano cha Redio Sengerema
mkoani Mwanza Bw. Felician Ncheye akiwakaribisha mameneja wa Redio za
jamii nchini walioshiriki kwenye mafunzo ya siku moja
ya kutoa elimu kwa Redio za jamii nchini juu ya kuandaa vipindi vyenye
ujumbe sahihi wa masuala yanayohusu watu wenye Albinism iliofanyika
katika kituo cha Redio Jamii Sengerema hivi karibuni. Katikati ni Afisa
mtetezi na ushawishi kutoka shirika linaloshughulika na watu wenye
Albinism la Under The Same Sun (UTSS), Kondo Seif na kulia ni Ofisa
Miradi ya Mawasiliano, Habari na Tehama wa Shirika la Kimataifa la
Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO) nchini, Al Amin Yusuph.

Ofisa Miradi ya Mawasiliano,
Habari na Tehama wa Shirika la Kimataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni
(UNESCO) nchini, Al Amin Yusuph akielezea dhima ya UNESCO kuwashirikisha
shirika la Under The Same Sun (UTSS) kutoa elimu kwa Redio jamii ili
kupaza sauti kwa jamii dhidi ya mauaji ya watu wenye Albinisim pamoja na
kutatua changamoto zinazowakabili walemavu wa ngozi.
Mshauri na Mkufunzi kutoka
Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Bi.
Rose Haji Mwalimu akitoa mwongozo kwa washiriki wa semina hiyo.
Afisa mtetezi na ushawishi kutoka
shirika linaloshughulika na watu wenye Albinism la Under The Same Sun
(UTSS), Kondo Seif akiendesha mafunzo kwa mameneja wa Redio jamii nchini
kwenye semina ya siku moja iliyofanyika wilayani
Sengerema mkoa wa Mwanza. Katikati ni Ofisa Miradi ya Mawasiliano,
Habari na Tehama wa Shirika la Kimataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni
(UNESCO) nchini, Al Amin Yusuph.
Meneja wa Redio jamii Mpanda FM
iliyopo mkoani Katavi, Prosper Kwigize akichangia maoni yake kwenye
semina hiyo namna ya kudhibiti mauaji ya watu wenye Albinism
iliyofanyika hivi karibuni wilayani Sengerema mkoa wa Mwanza.
Meneja wa kituo cha Redio Jamii
FADECO ya wilayani Karagwe, Adelina Lweramula akielezea jitahada za
kituo chake cha Redio kinavyoshiriki katika kukemea mauaji ya watu wenye
Albinism kwa kuendesha midahalo mbalimbali pamoja na makala maalum
kuhusiana na walemavu wa ngozi.
Baadhi ya mameneja wa vituo vya
Redio jamii nchini walioshiriki semina hiyo ya siku moja wakifuatilia
kwa umakini mafunzo yaliyokuwa yakitolewa na Bwana Kondo Seif wa Shirika la Under The Same Sun (UTSS).
Mkufunzi wa semina ya siku moja
kwa Mameneja wa Redio jamii nchini Kondo Seif akiwa kwenye picha ya
pamoja na baadhi ya washiriki wa semina hiyo.
Ofisa mtetezi na ushawishi kutoka shirika linaloshughulika na watu
wenye Albinism la Under The Same Sun (UTSS) Kondo Seif, ameitaka jamii
kuungana kupiga vita imani potofu zinazosababisha mauaji kwa watu wenye
albinism.
Alisema jamii ikiamka na kuamua kumaliza tatizo hilo, mauaji hayo yatakoma.
Kauli hiyo aliitoa katika semina ya siku moja ya elimu kwa Redio za
jamii nchini juu ya kuandaa vipindi vyenye ujumbe sahihi ya masuala
yanayohusu watu wenye Albinism iliofanyika katika kituo cha Redio Jamii
Sengerema mkoani Mwanza hivi karibuni.
Bw Kondo alisema katika jamii kumekuwa na imani potofu ambapo Albinism
wamekuwa wakiitwa majina yanayolenga kunyanyapaliwa na kusababisha
kushamiri kwa vitendo vya ukatili na mauaji dhidi yao.
Aliitaka jamii kutambua kuwa albinism ni hali ya ukosefu wa rangi
asilia mwilini inayoathiri ngozi, macho na nywele na ni nadra hali hiyo
kupatikana na haiambukizi kama watu wengine wanavyodhani.
Aidha ametaja jina sahihi la Kiswahili lililokubaliwa na baraza la
Kiswahili Tanzania kuitwa watu wenye albinism kuwa ni watu wenye
ualbino.
Alisema watu wenye ualbino wamekuwa wakikabiliwa na changamoto za
kukosekana kwa taarifa sahihi zinawagusa wao kama ngozi kushindwa
kuhimili jua, uoni hafifu na kupungua kwa usalama.
Kwa mujibu wa Takwimu za shirika hilo watu wenye Albinism zaidi ya
albino 70 nchini Tanzania wameuawa, zaidi ya 30 wamekatwa viungo vyao na
makaburi ya watu wenye Albinism 20 yamefukuliwa.
Ameviomba vyombo vya habari kushiriki kikamilifu kutoa elimu sahihi
kwa jamii ili kustawisha maisha ya watu wenye Albinisms kuwa kufanya
hivyo maendeleo yao, jamii na taifa kwa ujumla yataimarika.
Awali akizungumza na washiriki wa semina hiyo Ofisa Miradi ya
Mawasiliano, Habari na Tehama wa Shirika la Kimataifa la Sayansi, Elimu
na Utamaduni (UNESCO) nchini, Al Amin Yusuph aliwataka waandishi wa
habari kuzingatia matumizi sahihi ya lugha wanapoandika habari na
kuandaa vipindi vinavyozungumzia masuala ya Albinism.
Pia amesisitiza kuandaa vipindi vinavyobeba ujumbe sahihi wa
kuelimisha jamii juu ya masuala yanayohusu Albinism ili kubadilisha
mitazamo ya jamii ili kuwathamini, kuwalinda, kuwaheshimu na
kuwashirikisha katika maendeleo.
Sambamba na hilo amevitaka pia kubeba jukumu kubwa la kuhamasisha
wananchi kushiriki kikamilifu zoezi la uandikishaji katika daftari la
kudumu la mpiga kura na kutoishia kujiandikisha tu bali wajitokeze
kupiga kura kuwachagua viongozi ambao ni Madiwani, Wabunge na Raisi
October 2015 pamoja na kuipigia kura katiba inayopendekezwa wakati
ukifika.
Ameongeza katika matukio hayo muhimu ya kitaifa watu wenye Albinism
wahamasishwe kushiriki kikamilifu vile vile na makundi mengine kama
wanawake, vijana, watu wenye ulemavu, wazee na makundi mengine maalum.
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni