Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka amewataka Wakuu wa Shule zote mkoani Simiyu kuongeza ubunifu ili kuongeza ufaulu wa wanafunzi katika shule zao.
Aidha amesema kuwa wakuu wa shule wanatakiwa kuwa
wabunifu hususani katika mbinu mbalimbali zitakazosaidia kuwaandaa wanafunzi
vizuri kitaaluma ikiwa ni pamoja na mazoezi na mitihani ya kujipima ya
mara kwa mara, zitasaidia wanafunzi kufanya vizuri katika mitihani ya ndani na
ile ya kitaifa.
Mtaka ameyasema hayo wakati alipokuwa akifunga mafunzo ya
siku mbili kwa wakuu wa shule zote za Sekondari yaliyofanyika Mjini Bariadi
katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari Bariadi
“Kiongozi lazima uwe mbunifu, Mkiwa wabunifu
kwenye shule watoto watafanya vizuri,mnapaswa kubuni mbinu na mikakati
mbalimbali kwenye majaribio ya darasani, mitihani ya kujipima na kubuni
namna ya kuwapa motisha walimu wenu wapende kazi na kujiona ni wanafamilia
katika shule mlizopo” alisema Mtaka.
Aidha, aliwataka wakuu hao kujiwekea utaratibu wa kupita
mara kwa mara madarasani kukagua madaftari ya wanafunzi kwa lengo la
kujiridhisha, ikiwa walimu wanatimiza wajibu wao wa kuwafundisha kama
inavyotakiwa badala ya kusubiri kuletewa taarifa.
Mkuu huyo wa Mkoa pia aliwaasa wakuu hao kuwa na uongozi
shirikishi ambao unajali pande zote kwa maana ya walimu, wanafunzi na wazazi
ili waweze kujua kero na masuala mbalimbali yasiyowaridhisha na waweze kuchukua
hatua stahiki kwa mujibu wa taratibu kuyapatia suluhu.
Hata hivyo alisisitiza
wakuu wa shule kufanya vikao na wazazi kwa kuwa wazazi wanayo nafasi kubwa ya
kuchangia wanafunzi kufanya vizuri, hivyo akawataka wavitumie vikao kupata
maoni ya wazazi katika masuala mbalimbali ya kuboresha maendeleo ya wanafunzi
kitaaluma.
Aidha aliwataka Wakuu hao wa Shule kuzingatia sheria,
kanuni , taratibu na kuchukua hatua stahiki pale inapobidi ikiwa ni pamoja na
kutowaruhusu wanafunzi wajawazito au waliojifungua kuendelea na masomo.
Kwa upande wake Afisa Elimu wa Mkoa wa Simiyu, Mwl.Julius
Nestory alisema katika mafunzo hayo ya siku mbili wakuu wa shule wameelimishwa
juu ya sheria zote nne za Elimu, falsafa,nyaraka,kanuni mbalimbali za Elimu na
sera mpya ya Elimu.
wakuu hao walipewa mafunzo ya utunzaji wa nyaraka
za Serikali, udhibiti wa vitendo vya rushwa, kusimamia shule na taaluma pamoja
na utunzaji wa takwimu sahihi ambapo aliwataka wakuu wa shule hao kutumia
sheria zilizopo katika kusimamia shule kupitia mipango thabiti itakayotoa
matokeo chanya.
Naye Magebu Bugacha Mkuu wa Shule ya Sekondari Mwantimba
ameshukuru uongozi wa Mkoa kuona umuhimu wa kuwaandalia wakuu wa shule mafunzo
hayo ya kuwajengea uwezo ambayo yatawasaidia na kuwapa uzoefu katika kuendesha
na kusimamia shule zao.
Jumla ya Wakuu wa shule 152 kutoka katika Halmashauri
zote sita za Mkoa wa Simiyu wamepata mafunzo hayo ambayo yalilenga
kuwajengea uwezo katika usimamizi na uendeshaji wa shule za Sekondari.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni