Hatimaye Mashindano ya mbio za Baiskeli, yaliyohusisha washiriki
kutoka mikoa ya Mwanza, Simiyu na Arusha yamekamilika mkoani Simiyu, huku
mshiriki kwa upande wa wanaume kutoka Mkoa wa Arusha kuibuka mshindi na Mkoa wa
Mwanza ukitoa mshindi wa kwanza kwa upande wa wanawake.
Mashindano hayo ambayo kwa mara ya kwanza yameandika historia kwa
Mkoa wa Simiyu yalimalizika jana, huku idadi kubwa ya watu wakijitokeza
kushuhudia mbio hizo za baiskeli ambazo zilianzia eneo la Salunda na
kumalizikia katika viwanja vya Halmashuri ya Mji wa Bariadi.
Akizungumzia mashindano hayo, Mgeni rasmi wa mbio za baiskeli kwa
mwaka 2017, Naibu Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Tulia
Ackson amesema Mkoa wa Simiyu umeandika historia na kwamba mikoa mingine
ijufunze kutoka Simiyu, huku akitoa wito kwa wanawake kushiriki kwa wingi
kwenye michezo.
Tulia alisema kuwa michezo nchini haijapewa kipaumbele lakini
ikitumiwa vizuri inaweza kutoa ajira ukiwemo mchezo wa mbio za baiskeli; ambapo
ametoa wito kwa viongozi wa mikoa mingine pia kuwekeza katika michezo
mbalimbali ili kuwasaidia wananchi kupata kipato.
“Lililofanyika Simiyu ni jambo jema sasa hivi watu watakuwa
wanajua kuwa wakijifua vizuri kwenye baiskeli na ngoma za jadi wanakuja
kushiriki mashindano ya Baiskeli na ngoma Simiyu, nitoe wito kwa viongozi
wengine kufikiria mambo mengine yanayoweza kuwasaidia wananchi katika maeneo
yao kupata ajira na kujipatia kipato” alisema.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka amesema mkakati wa mkoa huo
ni kurasimisha tamaduni zote na kuhusianisha na shughuli za Utalii ndani ya
mkoa huo.
“ wasanii wote watatambuliwa na baadae kujengewa uwezo
kupitia watalaam wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(Kitivo cha sanaa),Chuo cha
Sanaa Bagamoyo na vyuo vya michezo ili waweze kufanya kazi zao kibiashara na
kuimarisha uchumi wao” alisema Mtaka.
Wakizungumzia ushindi baadhi ya washiriki kutoka Simiyu, Arusha na
Mwanza walisema hiyo ni fursa nzuri ya kujiandaa kwa mashindano makubwa na
kwamba wadhamini waendelee kujitokeza kudhamini michezo kama hiyo.
Mashindano hayo yalidhaminia na Jambo food products ambapo mshindi
wa kwanza kundi la wanaume waliokimbia km 200 alijinyakulia zawadi ya pikipiki yenye
thamani ya sh milioni mbili Khamis
Hussen kutoka Arusha mshindi wa pili Masunga Duba kutoka simiyu na kujinyakulia
kiasi ya pesa milioni moja(1,000,000,000) na mshindi wa tatu Richard Raiza
kutoka arusha ambaye alijipatia laki tano.
Upande wa wanawake mshindi wa kwanza alikuwa Laulencia Mtuba
kutoka mwanza na kujinyakulia laki tano,mshindi wa pili Tatu Charles Kutoka
mwanza ambaye alijipatia shilingi laki nne huku mshindi wa tatu Vumilia
Msinambula kutoka simiyu na kuambuli shilingi laki tatu.
Watu wenye walemavu
waliokimbia km 5 mshindi wa kwanza Emmanuel Mtemi ambaye alijinyakulia shilingi
laki mbili,mshindi wa pili Masunga Sendema ambaye alichukua shilingi laki moja
na nusu,huku mshindi wa tatu Saguda Sospeter ambaye alijinyakulia shilingi laki
moja.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya Jambo Food
Products,Mhe.Salum Khamis ambaye ndio Mdhamini wa mashindano ya Baiskeli na
ngoma za Asili (Simiyu Jambo Festival) amesema ataendelea kudhamini mashindano kama
hayo Mkoani Simiyu ili kuwawezesha wananchi kuinua kipato kupitia vipaji vyao.
Na ANITA BALINGILAKI
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni