MKUU wa Mkoa wa simiyu Antony Mtaka amewahamasisha wananchi kuendelea kulima zao
la pamba kwa kuwa Serikali imekusudia kujenga kiwanda cha bidhaa za Afya
zitokanazo na zao hilo mkoani humo na wataalam wanaofanya upembuzi yakinifu wanatarajia
kufika Mkoani Simiyu Septemba 20 mwaka huu kuona eneo kitakapojengwa kiwanda.
Mkuu huyo amesema wananchi wasikate
tamaa kulima pamba kwa sababu ya matatizo ya kihistoria na kuwaeleza, Serikali
ya Mkoa imeweka mikakati madhubuti ya
kuirudisha pamba kuwa dhahabu, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wananchi wanapata
pembejeo, mbegu bora, dawa, na suala la bei ya pamba itaanza kujadiliwa mapema.
Hata hivyo amewataka wakulima wasiache kulima mazao jamii ya mikunde
hususani choroko na dengu kwa kuwa Serikali inashughulikia suala la upatikanaji
wa soko la uhakiki pamoja na kupunguza au kuondoa kabisa madalali katika
biashara ya mazao hayo ili wananchi wanufaike kupitia kilimo.
Akitolea ufafanuzi hoja ya Diwani wa
Kata ya Ikungulyabashashi.Bupi Maduhu Litunga ya kupimiwa maeneo, Mkuu huyo wa
Mkoa amemuagiza mkurugenzi mtendaji
wa halmashauri ya Wilaya Bariadi kupitia
Idara ya Ardhi, kuitisha mikutano katika Vijiji vyote ambavyo wananchi
wanahitaji kupimiwa maeneo na baadae awasilishe mihutasari ya vikao hivyo
Ofisini kwake tarehe 13/09/2017.
Katika hatua nyingine Mtaka amepiga
marufuku Halmashauri zote Mkoani humo kutoza ushuru wa biashara ndogondogo
zinazofanywa na wananchi kwa kutandika na kupanga bidhaa zao chini au kuuzwa
katika mabeseni maarufu kama matandiko.
Amesema suala hilo lilishatolewa
maelekezo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Pombe Magufuli,
hivyo Halmashauri zinapaswa kubuni vyanzo vipya vya mapato vyenye tija kwa
Halmashauri badala ya kutegemea kutoza ushuru unaowakwaza wananchi.
Hata hivyo ameitaka Halmashauri ya
Wilaya ya Bariadi kuhakikisha inarejesha asilimia Kumi ya mapato
yanayokusanywa kutoka katika vijiji vyote kwenye kila robo mwaka ili Vijiji
hivyo viweze kutekeleza mipango ya maendeleo iliyowekwa.
Mtaka ametoa agizo hilo wakati wa
ziara yake wilayani Bariadi yenye lengo la kusikiliza kero za wananchi na
kuzitafutia ufumbuzi .
“Kama kuna Halmashauri bado inatoza
ushuru wa matandiko wamechelewa sana, kuanzia kesho hamna huo ushuru, kama
mnafikiri mapato ni kutoza tandiko la dagaa…mchicha poleni kama wakuu wa
idara hiki ndicho chanzo mnachokifikiria kichwani hiyo kazi haiwafai, mkatafute
kazi nyingine za kufanya” alisema Mtaka.na kuongeza kuwa:
“. Sasa mtu anahangaika na
beseni lake la nyanya wewe unamtoza ushuru, umechangia nini, beseni si lako
nyanya si zako” alisema Mtaka.
Mtaka amekamilisha ziara yake katika
Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi ambapo amesikiliza na kutatua kero za wananchi
katika sekta ya Elimu,Afya, Kilimo, Mifugo, Ardhi, Ujenzi, Biashara na Uchumi
pamoja na suala la utekelezaji wa Mradi wa Umeme Vijijini (REA) ambazo
amezitolea maelekezo na ameahidi kufuatilia utekelezaji wake.
Na ANITA BALINGILAKI
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni